loader
Picha

Uwekezaji katika teknolojia ya mawasiliano kwa wanawake ni muhimu

Hata katika ngazi za vyuo vikuu hapa nchini wavulana ndio wanaonekana kuvutika zaidi katika kusomea masomo ya teknolojia hiyo huku wasichana idadi yao ikiwa ni ya chini.

Mwasisi wa Shirika lisilokuwa la kiserikali la Apps and Girls, Carolyne Ekyarisiima anasema kuwa wakati alipokuwa akisoma katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala, (KIU), msukumo wa wasichana kujiunga kwenye masomo hayo ya Teknolojia na Mawasiliano ulikuwa mdogo.

Katika darasa la wanafunzi 50 wasichana walikuwa ni wachache sana walifika hadi wanafunzi watano tu. Anasema kuwa sio kwamba wasichana hawafahamu au hawawezi masomo hayo ila ni ile hali ya kutokuwa na msukumo wa ziada wa kuwasaidia kupenda masomo hayo.

Anaongeza kuwa sababu inaweza kuwa imeanzia chini kabisa kwenye msingi wa masomo hayo wakati wa ngazi za elimu ya shule za msingi au sekondari. Carolyne anaongeza kuwa shule nyingi hakuna vifaa vya kutosha vya kusomea masomo hayo na hivyo kwa wale wavulana ambao wanakuwa na ujanja wa kupenda fani hiyo hutumia muda wao hata katika kutafuta kompyuta mitaani.

“Mimi naona kuwa wasichana wengi sio kwamba hawana uwezo wa masomo haya, hapana ila kunakuwa na sababu nyingi kama vile mazingira yanayowazunguka na mengineo lakini je, vipi kama kwenye fani nyingine kama udaktari na nyinginezo si wasichana wanafanya vema watashindwaje huku?” Anahoji Carolyne.

Anaongeza kuwa “hakuna tatizo kwenye masomo ya sayansi kwa wasichana kwa kuwa yanawapendeza na yanaweza kubadilisha mfumo mzima wa maisha yao katika jamii kwa ujumla.” Carolyne ni mwanafunzi wa Shahada ya Uzamili katika chuo hicho cha Kampala lakini pia ni mwanaharakati ambaye ana nia nzuri ya kubadilisha fikra mbaya zinazosababisha ushiriki hafifu wa wanafunzi wa kike katika masomo hayo.

Akiwa anadhaminiwa na Kampuni ya simu za mkononi ya Tigo, Carolyine kupitia shirika lake hilo anatoa mafunzo ya bure kwa wanafunzi wa kike wa sekondari mbalimbali nchini. Ameshawafikia wanafunzi wa sekondari mbalimbali za Dar es Salaam ambapo wamepewa elimu ya matumizi ya kompyuta.

Wanafunzi hao wanapatiwa mafunzo hayo ya siku moja ambapo wanatumia laptop mbalimbali katika kutoa mafunzo hayo. Anasema kuwa wanafunzi wanafundishwa namna bora ya utengenezaji wa tovuti kwa kiwango chenye ubora zaidi. Anaongeza kuwa wanafunzi waliohusika ni kutoka sekondari za Kisutu, Jangwani na ambao wana umri wa miaka 14 hadi 18.

“Wanafunzi hawa wanachohitaji ni kuandaliwa mazingira bora ya kupenda kompyuta na hapa sio tu kompyuta kama kifaa ila hata yale yote yanayotokana na kompyuta hizo ikiwa ni pamoja na utengenezaji wa tovuti pamoja na gazeti tando kwa kuwa huko nako kuna fedha nyingi zinazoweza kupatikana kwa namna mbalimbali,” anasema Carolyne.

Anaongeza kuwa “fedha zinaweza kupatikana nyingi tena sana tu kwa njia hizi za tovuti na gazeti tando kulingana na ubunifu utakaotumika.” Carolyne amewahi kushinda fedha za mradi wa Tigo ambao unahusiana na kudhamini watu wanaosababisha mabadiliko katika jamii kwa njia ya teknolojia.

Alijishindia Dola za Kimarekani 25,000 ambazo amezitumia katika kuwafundisha wanafunzi mambo mbalimbali kuhusiana na teknolojia. Kwa upande wake Mhadhiri msaidizi wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala (KIU), Wilheim Oddo ambaye ndio mfundishaji mkuu wa mafunzo hayo akiwa chini ya shirika hilo pia anasema kuwa wasichana wanaweza kuwa ni hazina kubwa ya maendeleo yatokanayo na teknolojia.

Anaongeza kuwa kwa kipindi ambacho amekuwa akiwafundisha wanafunzi wa shule mbalimbali masuala hayo amegundua kuwa wengi wao wana vipaji vikubwa. Anafafanua zaidi kuwa kwanza inatakiwa kuwa na mapenzi ya fani hiyo na kisha kuanza kuwa na mikakati ya kujifunza mengi ili kuongeza ufanisi.

Pia anawataka wasichana kutambua kuwa kuna utajiri mkubwa katika teknolojia ambao unaweza kuwaongezea vyanzo vya mapato hata wakati wakiwa bado wanafunzi. “Hakuna ubishi katika hili kwa kuwa wanafunzi wanaweza kujipatia fedha nyingi hata wakati wakiwa bado wanaendelea na masomo yao,” anasema Oddo.

Anaongeza kuwa “wakishaweza kuandika habari zao katika mitandao na kisha wakaweza kutafuta picha na kuandika masuala mbalimbali yatakayokubaliwa na kuwafanya wanafunzi wenzao watembelee blogs au tovuti zao basi wataweza hata kuanza kupata matangazo ya biashara.”

Kwa upande wake Meneja wa Uwajibikaji kwa Jamii kutoka Kampuni ya Tigo ambayo ni wadhamini wakubwa wa mradi huo, Woinde Sishael anasema kuwa wanafunzi wanaweza kuwa ni moja kati ya wadau wakubwa wa teknolojia ya mawasiliano. Anafafanua kuwa wanafunzi wengi wanatumia mitandao ya kijamii kama vile, Facebook, Twitter na mingineo na wanatumia kupata habari mbalimbali.

Anaendelea kuwa kinachotakiwa kwa sasa ni kuwaweka karibu wanafunzi na teknolojia yenyewe kwa kuwaelekeza ni kwa kiasi gani wanaweza kupata fedha kwa njia ya mitandao hiyo. Anafafanua kuwa wanawasiliana kwa mitandao hiyo na kuongeza idadi ya marafiki ila wanakuwa zaidi wanatumia simu zao za mkononi.

“Kwa kufundishwa kwao namna bora ya utengenezaji na uendeshaji wa hizi tovuti za kwao ambazo wanaweza kuzifungua na kuziendesha wenyewe itasaidia kwa kiasi kikubwa wao kuziona fursa na kuzitumia katika kupata fedha,” anasema Woinde. Anaongeza kuwa “wanafunzi wengi wapo kwenye facebook na huko pia kuna namna ya wao kunufaika na mitandao hiyo na ile mingineyo kwa manufaa zaidi na sio tu kwa kuwa na marafiki peke yake.”

Mmoja kati ya wanafunzi waliowahi kushiriki mafunzo hayo, Jasmine Nzowa anasema kuwa mafunzo hayo yamemfungua mawazo kuhusiana na namna ya matumizi ya kompyuta na faida zake. “Mimi ninataka nikimaliza kidato cha sita nianze kwenda kusomea zaidi masomo haya na kuondokana na ile dhana ya kuwa haya ni masomo ya wanaume zaidi,” anasema Jasmine.

WAKULIMA zao la korosho mkoani Lindi wamelipwa Sh bilioni 85 ...

foto
Author: Evance Ng’ingo

Recent Posts

Categories

more headlines in our related posts

latest # news