loader
Picha

Mrembo anayetetea maisha ya watoto njiti

Doris (Kulwa) ambaye ni pacha wasiofanana, mwenzake anaitwa David Mollel (Doto), walizaliwa njiti miaka 24 iliyopita mkoani Arusha, katika familia ya William Mollel (sasa marehemu) na Mama Celina Mollel, wakiwa ni uzao wa kwanza kwenye familia hiyo ya watoto watatu.

Kilichopo ndani ya Doris ni kikubwa, kwani kwa umri wake huo wa miaka 24, tayari ana elimu ya Stashahada ya Uzamili ya Utawala wa Mahusiano ya Kimataifa na pia ni mwanafunzi wa Shahada ya Uzamili katika Chuo Kikuu cha Mzumbe, akisoma Masuala ya Utawala na Uongozi.

Akizungumzia moyo wake wa kupenda kusaidia wasio na uwezo, Doris ambaye pia anashikilia taji la urembo kutoka Singida na pia mrembo wa Tanzania hivi sasa katika nafasi ya tatu, anasema moyo wa kutoa uko ndani yake tangu mdogo.

“Nikiwa mdogo nadhani sijaanza shule ya msingi, nilikuwa nachukua vitu kwenye friji, napelekea watoto wenzangu wasio navyo...nilifanya hivyo kwa kujificha wazazi wasinione,” anasema Doris. Tabia hiyo hakuiacha kwani aliona si vyema wao wawe na vyakula vingi kwenye friji wakati wapo watoto wa jirani hawana chakula na tabia hiyo aliendelea nayo hadi alipofika sekondari, chuo na hata mpaka leo.

“Nilijiunga na elimu ya sekondari katika shule ya Umoja, ambako nilikuwa natoa vitu kwa watu... nilikuwa napita bwenini kukusanya vitu kutoka kwa wanafunzi wenzagu na kupelekea watu wasio na uwezo katika kijiji cha jirani na shule hiyo,” alisema Doris.

Tabia hiyo hiyo kwa Doris si ya kuiga kwa mtu, au kufanya kwa kutafuta sifa, hapana ni jambo lililo ndani ya moyo wake na anapenda kutoa kwa wahitaji ndio maana anafanikiwa katika mambo yake.

Msichana huyo, unaweza kumuona ni mtu wa pekee katika jamii, kwa sababu ana tabia ambazo si rahisi kwa wasichana walimbwende kama yeye kuwa na moyo huo wa kupenda kutoa bila kulazimishwa.

Kutoa kwa Doris ni kitu cha ajabu, kwani anaweza kutoa hadi senti yake ya mwisho mfukoni kwa mhitaji atakayemuona, na hiyo imemfanya awe mtu wa kujali muda.

Hakuishia kutoa tu, kwani alipomaliza elimu ya sekondari kidato cha sita mwaka 2011, mwaka uliofuatia, alishiriki mashindano ya urembo akiwa Chuo Kikuu cha Mwalimu Nyerere akisoma Shahada ya kwanza ya Siasa na Usimamizi wa Maendeleo ya Jamii.

Alifanikiwa kutwaa taji la mrembo wa Utalii Juni mwaka 2012, na kitu cha kwanza kufanya baada ya kuchaguliwa huko, ni kupeleka watoto yatima wa kituo cha Chakuwama, Sinza, Dar es Salaam kwenda kuona vivutio vya utalii mjini Bagamoyo.

“Niliona ni vyema nitangaze utalii na niliona ni fursa nzuri ya watoto hao kwenda kuona vitu vya kihistoria, kwa sababu kwa hali ya kawaida wasingeweza kwenda kutokana na kukosa uwezo,” alisema Doris.

Hakuishia hapo, mwaka 2013 alishiriki mashindano mengine ya mrembo wa Tabata na kuwa Mrembo wa Ilala ambako nako alishinda na alichofanya ni kusaidia watoto wa shule za msingi vitabu vya kiada na ziada.

Alipata ufadhili huo kupitia Shirika la Mkuki na Nyota, ambao walimpa vitabu 100 kwa kila shule kati ya shule saba alizopeleka vitabu hivyo. Pamoja na kuwa mrembo huyo, aliona bado ana kitu cha kufanya na ndipo akaenda Msimbazi Centre, jijini Dar es Salaam kwenye Chuo cha Mafunzo ya Uhazili, ambako aliomba kupewa muda wa dakika chache awafundishe wanafunzi hao ujasiriamali.

“Niliona nina kitu cha kusaidia wanafunzi hao, niliomba na kupewa dakika 40, kufundisha masuala ya ujasiriamali,” anasema Doris.

Alifanya hivyo kwa muda na mwaka 2014, alishiriki mashindano ya mrembo wa Singida na kushinda na kazi ya kwanza kufanya kwenye jamii ni kusaidia jamii ya Wahadzabe ambapo hupeleka mahitaji kama vile vitabu na mashuka.

Jamii hiyo imehamasishwa kupeleka watoto wao shule, ambako wanasoma kwenye Shule ya Msingi Munguli ambayo ni ya bweni, na yeye alitumia nafasi yake ya mrembo na moyo wake wa kutoa, kusaidia kupeleka vitabu. Aidha Doris pia amesaidia Shule ya Kindai kujenga matundu 18 ya choo kwa kushirikiana na aliyekuwa Mbunge wa Singida, Mohamed Dewji.

Anasema ujenzi huo ulifanywa kwa kuwa shule hiyo ilikuwa na changamoto ya choo, jambo ambalo lilisababisha wanafunzi na wazazi kukaa kwa tabu shuleni hapo. Akiwa mrembo kutoka Kanda ya Kati, pia alisaidia shule za Dodoma ikiwemo Shule ya Msingi Mpunguzi, ambayo aliipa vitabu 250, alivyopata kwa msaada wa kampuni ya Marks Solution. Baada ya kufanya yote hayo katika jamii, Doris aliona ni vyema afungue taasisi ya kusaidia watoto njiti, kwani hata yeye na pacha wake walizaliwa njiti na huduma bora za afya ndizo zinazoweza kusaidia watoto hao waishi.

“Mwaka huu Machi nilifungua Taasisi ya Doris Foundation, inayosaidia watoto njiti na mama zao, niliona ninawiwa kufanya hivyo kwa sababu watoto hao wengi hufa kwa kukosa huduma,” anasema Doris.

Jambo la kwanza alilofanya Doris ni kununua mashine nne pamoja na vifaa tiba na vya kulishia watoto hao katika Hospitali ya Mkoa ya Singida na fedha za kununua machine hizo alizipata kupitia fomu ya mchango aliyochangisha watu mbalimbali. Doris ni msichana wa ajabu, anayeona mbali, si mwoga pia ni mtu anayeweza kushawishi na kusimamia jambo lake, asiyependa kukatishwa tamaa na ndio siri kubwa ya mafanikio yake.

Kupitia taasisi hiyo, amepata ufadhili kutoka Kampuni ya Vodacom ambayo imemsaidia kwenye hafla mbalimbali za kuchangisha na kupata fedha kwa ajili ya kununua mashine kwa ajili ya kusaidia watoto njiti. Katika ufadhili huo na Vodacom, Doris alifanikiwa kuchangisha fedha zilizonunua mashine nne, zikiwemo za hewa ya oksjeni na zile za kunyonya uchafu watoto hao wanapozaliwa.

Vifaa tiba hivyo mashine moja ikiwa na gharama ya Sh milioni 3.5, viligawiwa katika hospitali tatu za jijini Dar es Salaam, ambazo ni Mwananyamala, Amana na Temeke. “Unajua mtoto njiti akifa ni kwa kukosa huduma bora ya afya, wakitunzwa vizuri wanapona na hata sisi tumepona kwa sababu tulipata huduma bora ya afya, sasa si vizuri watoto hao wafe, tunaweza kuwasaidia wapone na kuishi kama sisi,” alisema Doris.

Doris amefanya mengi kusaidia jamii na watu wenye mahitaji wakiwemo wazazi wanaojifungua watoto njiti, ambapo alisimamia kazi ya kuchangia damu kwa ajili yao katika Siku ya Wanawake Duniani, ambapo alipata uniti 65. Pia Siku ya Damu Duniani, alishiriki kuhamasisha watu kujitolea damu eneo la Ukonga, ambapo walifanikiwa kupata uniti 14.

Lakini pia hajasahau watu wa Zanzibar, kwani nako amefika kwa kuwapa msaada wa mashine tatu za kusaidia watoto njiti. Kupitia taasisi yake hiyo, Doris alifanya kampeni ya watoto njiti ambayo aliianza Novemba mwaka huu katika Hoteli ya Kilimanjaro Kempisk akishirikiana na wadau wengine, lengo likiwa kupata mashine 80 za kunyonyea uchafu watoto njiti pamoja na mashine za oksijeni.

Anasema vifaa vitakavyopatikana vitagawanywa katika kanda nane nchini ambapo kila kanda ingepata mashine 10. Katika kampeni hiyo walifanikiwa kupata mashine kadhaa na vifaa tiba ambavyo vitaanza kugawanywa katika mikoa kadhaa ikiwemo, Iringa, Manyara, Mtwara na Mara.

Hata hivyo Novemba 26, mwaka huu Doris alianza safari ya kwenda mikoa hiyo kugawa mashine hizo na kampeni ya kuendelea kuchanga fedha za kununua mashine hizo inaendelea, ili kuhakikisha watoto njiti nchini hawafi kwa kukosa huduma za afya.

“Tuna matarajio makubwa, tunataka kuona katika hospitali zetu kuna wodi za akinamama wanaojifungua watoto njiti, ili kupunguza vifo vya watoto hao ambavyo vingi vinatokana na kukosa huduma tiba,” anasema Doris. Doris anaweza kufanya hayo yote kwa kuwezeshwa na Mungu, kwani anaamini bila msaada wa Mungu asingeweza kufika hapo alipo. Ukiangalia mambo anayofanya msichana huyo ni mengi, kusoma, kufanya kazi na kusafiri.

“Kwa kweli napanga muda wangu, wakati mwingine inanilazimu kuacha kufanya mitihani kwa ajili ya kufanya kazi za jamii, na mitihani hiyo huwa nakuja kuifanya baadaye kama mitihani maalumu, ila namshangaa Mungu ninafanya vizuri,” anasema Doris.

Doris anaishi nyumbani kwao Kimara na mama yake na anasema hategemei kuhama hadi hapo atakapoolewa, kwani ana mchumba ambaye anamshauri na kumsaidia katika harakati zake za kusaidia jamii.

Huyo ndiye Doris Mollel, mlimbwende mwenye umri mdogo anayefanya mambo makubwa na mazuri katika jamii, je wewe mwenye umri sawa na huyo umeifanyia nini jamii yako?

WAKULIMA zao la korosho mkoani Lindi wamelipwa Sh bilioni 85 ...

foto
Author: Ikunda Erick

Recent Posts

Categories

more headlines in our related posts

latest # news