loader
Picha

JOYCE KIRIA: Staa wa luninga aliyekanyaga Jiji la Dar akiwa hausigeli

Kwa mujibu wa mtangazaji maarufu wa kipindi cha Wanawake Live na Mkurugenzi wa taasisi ya Haki za Wanawake (HAWA), Joyce Kiria baada ya kufanya mahojiano na gazeti hili hivi karibuni anasema yeye ni mmoja kati ya watoto wengi ambao hawakuweza kupata elimu kutokana na changamoto hiyo ingawa alikuwa na uwezo mkubwa darasani.

Kiria, mtoto wa kwanza kati ya watoto saba wa Mzee Emmanuel Kiria ambaye sasa ni marehemu na mama Tharisila Mboya alizaliwa Desemba 1980 Marangu Mkoa wa Kilimanjaro. Anasema aliweza kupata elimu ya msingi katika Shule ya Nkonyaku na kumaliza darasa la saba mwaka 1996 hata hivyo hakuweza kuendelea na masomo ya sekondari kutokana na uwezo wa wazazi wake kutoruhusu kumsomesha zaidi.

“Kutokana na hali ya maisha ya nyumbani sikuweza kuendelea kusomeshwa masomo ya sekondari mama alinitaka kuja mjini Dar es Salaam kufanya kazi za ndani,” anasema Kiria. Kiria anasema mama yake alimtaka kuja Dar es Salaam kufanya kazi za ndani baada ya mama mmoja kwenda kuomba msichana wa kumsaidia kazi za nyumbani ambaye alikuwa akiishi Kimara.

Anasema baada ya kufika mjini na kuanza kazi za ndani, maisha hayakuwa rahisi kutokana na kazi nyingi alizokuwa akifanya mbali na kazi za usafi, kufua na kupika pia ilimbidi kuhudumia kuku kwa kuwa mama huyo ambaye ni bosi wake alikuwa ni mjasiriamali ambaye alikuwa akifuga kuku.

“Nilifanya kazi hiyo kwa karibu miaka miwili nikijitahidi kutunza fedha nilizokuwa nikipata.... nilikuwa nikilipwa Sh 5,000 kwa mwezi, nilikuwa sifurahii kufanya kazi hiyo, kilichokuwa kikiniumiza zaidi ni mama niliyekuwa nikimfanyia kazi alikuwa na watoto wa umri wangu ambao nilikua nikiamka kuwaandaa kwenda shule wakati mimi sina uwezo wa kwenda shule,” anasema.

Anasema toka akiwa shule alikuwa akipenda sana kusoma na ndoto yake ilikuwa kusoma sana ingawa hakuwa anajua atakua nani katika maisha yake. “Darasani nilikuwa nikijitahidi sana natoka mtu wa kwanza au wa pili nikishuka kidogo nalia sana na nilipomaliza darasa la saba nilifaulu kwenda sekondari lakini wazazi hawakuwa na uwezo wa kutimiza ndoto yangu ya kuwa msomi,” anasema Kiria.

Baada ya hapo anasema aliamua kuacha kazi hiyo na kwenda kwa mama yake mdogo ambaye alikuwa akiishi eneo la Urafiki akamuomba aishi naye wakati akitafuta kazi wakati huo akiwa na umri wa miaka 18, baada ya kupita pita akitafuta kazi aliweza kupata kazi kama kibarua katika kiwanda cha mablangeti kilichopo Chang’ombe akilipwa Sh 30,000.

Anasema aliamua kuondoka kwa mama yake mdogo kwenda kupanga Ilala ambako chumba alikuwa akilipa Sh 5,000 baada ya kuona Urafiki ni mbali na anakofanya kazi. Baada ya kuhamia Ilala alikuwa akitembea kwa miguu kwenda kibaruani kwake Chang’ombe. Hakuweza kufanya kazi hiyo kwa muda mrefu kutokana na kusumbuliwa na kifua kutokana na vumbi la mablangeti.

Anasema fedha alizokuwa akizipata aliamua kuanzisha biashara ya kutengeneza sambusa baada ya kufundishwa na mama mmoja ambaye pia alimtambulisha ofisi mbalimbali alizokuwa akiuza na yeye kuanza kufanya kazi hiyo akiuza katika kituo cha redio cha Clouds na ofisi nyingine jengo la Kitega Uchumi (katikati ya Jiji) na benki zilizo karibu.

“Yule mama tayari alikuwa na soko lake, kwa kuwa aliamua kuacha kazi hiyo alinionesha maeneo yake kwa hiyo nikawa asubuhi napika sambusa na kupeleka huko kuuza kila siku, nilikuwa nikiuza sambusa 100 hadi 120 kwa siku..... katika jengo hilo sasa nilifahamiana na watangazaji mbalimbali wa redio hiyo,” anasema Kiria.

Anasema kazi hiyo ya kupika sambusa na kuuza pia hakuifanya kwa muda mrefu kwa sababu alianza tena kusumbuliwa na kifua na kuamua kuacha, hivyo alihangaika tena na kupata kazi ya kuuza duka Kariakoo kazi ambayo aliifanya kwa mwaka mmoja. Anasema alikusanya fedha alizopata na kufungua kibanda chake cha kupigisha simu Ilala, karibu na Chuo cha Uandishi wa Habari Dar es Salaam (DSJ) mwaka 2001.

“Eneo lile lilikuwa na wasichana wengi na mimi kwa sababu nilikuwa nimefanya kazi Kariakoo nilikuwa najua nguo nzuri hivyo nilikuwa navaa vizuri wanafunzi wakiniona wanapenda nguo zangu nikapata wazo la kuingia Kariakoo nanunua nguo naweka kwenye kibanda changu nauza,” anasema Kiria.

Anasema biashara hiyo ilikuwa ikimlipa zaidi ya mara mbili ambapo kati ya wateja wake alikuwa ni Mbunge kijana marehemu Amina Chifupa ambaye alikuwa akisoma katika chuo hicho wakati huo, pamoja na watangazaji na waandishi wa habari wengine.

Anasema alianza kuvutiwa na kazi ya habari na hasa utangazaji, alijaribu kwenda kuuliza katika chuo kile cha DSJ ili aweze kujiunga na masomo lakini alishindwa kutokana na vigezo vilivyomtaka kuwa na cheti cha kidato cha nne wakati yeye aliishia darasa la saba na hata cheti hakuchukua baada ya mama yake kumpeleka Dar es Salaam kufanya kazi za ndani.

“Kwa sababu nilikuwa nimeshawazoea wafanyakazi wa radio Clouds niliamua kwenda hapo kuomba kujifunza, hawakunikatalia baada ya kuwaambia kuwa nina ndoto ya kuwa mtangazaji maarufu, nikaanza kufanya mazoezi bila kulipwa,” anasema Kiria.

Anasema akiwa katika mafunzo ya kuandaa na kuendesha vipindi aliweza kubuni vitu mbalimbali na baadaye alianzisha Movie leo na baadaye kipindi cha Bongo Movie katika Televisheni ya Channel Ten na baadaye kuhamishia East Africa TV ambacho alikuwa akizungumzia mambo mbalimbali ya filamu za hapa nyumbani.

Kiria anasema alibahatika kuolewa ndoa ya kwanza ambayo hakudumu kwa muda mrefu kutokana na changamoto mbalimbali zilizompelekea kupata wazo la kuanzisha taasisi ya kutetea haki za akinamama.

Anasema baada ya kupata changamoto hizo alikwenda katika vituo na taasisi mbalimbali zinazoshughulikia mambo ya wanawake lakini hakuweza kupata msaada hivyo aliona kuna haja ya kina mama kupata chombo cha kutatua matatizo yao na pia sehemu ya kusemea.

“Niliamua kuanzisha taasisi ya HAWA kuwapa sauti wanawake kujadili changamoto zao, kutafuta suluhu na pia kuangalia fursa mbalimbali kwa pamoja na kuzitumia, nikaanzisha na kipindi cha Wanawake Live ambacho kinajadili masuala ya wanawake.”

Anasema kwa kushirikiana na vituo mbalimbali vya sheria ameweza kuwasaidia wanawake mbalimbali mijini na vijijini, kupitia wataalamu wengine ameweza kutoa mafunzo kwa akinamama ili waweze kujimudu na kuachana na utegemezi kwa waume zao. “Wanawake wengi ni goli kipa, hawana uwezo wa kujiingizia kipato chochote wanasubiri wanacholetewa na waume zao, inapotokea tatizo au migogoro ndani ya nyumba inakuwa tatizo,” anasema Kiria.

Anasema wanawake kutokuwa na uwezo kiuchumi ni mwanzo wa migogoro mingi ndani ya ndoa na pia hawaheshimiki ndio maana HAWA inasimama na kuwapatia elimu ya ujasiriamali na pia kuwaongoza kupata mikopo katika vikundi kupitia kaulimbiu za ‘ndoano’ na ‘mwanamke jipe shughuli’.

Hata hivyo Kiria anasema kuwa changamoto kubwa anayoipata sasa katika shughuli zake ni elimu, anasema mambo mengi yanamtaka awe na upeo mkubwa wa kupambanua jambo ambalo ni tatizo kwake kutokana na elimu aliyonayo.

“Nina mpango wa kurudi shuleni nipate elimu ya sekondari na baadaye kuendelea lakini sasa ndoto yangu kuu ni kuwahudumia akinamama, kuanzisha televisheni ya kinamama, matatizo ya wanawake ni mengi kipindi cha masaa machache hakitoshelezi.” Kiria baada ya ndoa ya kwanza kuvunjika sasa ameolewa na Katibu wa Chadema Mkoa wa Dar es Salaam, Henry Kilewo na ana watoto wawili Linstone na Lincon.

Anasema changamoto ambayo amewahi kukumbana nayo katika safari yake ya maisha kuna wakati aliishi gerezani kwa karibu mwezi mmoja baada ya aliyekuwa rafiki yake wa kiume kumshtaki kuwa amemwibia dhahabu, hata hivyo aliachiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya mtu huyo kukimbia baada ya madini hayo kugundulika kuwa sio halisi.

Huyo ndiye Joyce Kiria. Je, ataendelea kujiondoa katika unyonge aliokuwa nao, huku akiwasaidia wanawake wengine kujikwamua kielimu, kiuchumi na nyanja nyingine katika jamii? Tusubiri.

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameahidi kupokea kundi la watalii wasiopungua ...

foto
Author: Regina Kumba

Recent Posts

Categories

more headlines in our related posts

latest # news