loader
Picha

HOYCE TEMU: Mrembo wa Tanzania aliyefanikiwa filamu Rwanda kuepuka kashfa katikati ya umaarufu

Hoyce ni mmoja wa warembo ambao wamekuwa wakijiweka mbali na skendo, ingawa kuna baadhi ya watu wamekuwa wakimchafua kwenye mitandao ya kijamii na kutokana na mafanikio ya kuendeleza sanaa ya urembo bila kashfa, gazeti hili lilimtafuta na kufanya naye mahojiano. Swali: Ukiwa ni maarufu unawezaje kudhibiti skendo?

Jibu: Unajua umaarufu unatafutwa kwa njia nyingi, umaarufu ni gharama, kuupata ni kazi lakini kuushusha ni rahisi sana, kiukweli umaarufu wangu niliupata kwa kutwaa taji la Mrembo wa Tanzania mwaka 1999 na kupeperusha bendera ya nchi, ni taji kubwa sana. Jamii inaniangalia mimi nataka kuwa mfano mzuri wa kuigwa kwa kusaidia jamii yangu ya Tanzania, naweza kusema kikubwa ni kujitambua na kutambua thamani yangu.

Swali: Unazungumziaje skendo za mastaa wa kike?

Jibu: Vidole havilingani, binadamu tumetofautiana, kuna warembo wanaingia kwenye Miss Tanzania kwa jicho la jamii na wengine kwa jicho la mimi kwanza, hilo ndio baya. Unakuta wanafanya vitu vya ajabu kwa kujiingiza kwenye maskendo na kutaka fedha za haraka. Umaarufu sio skendo ukifanya kitu kizuri cha kupendeza jamii lazima utapata umaarufu, lakini wengine wanatafuta umaarufu kupitia mitandao kwa kupiga picha za utupu, warembo ambao wameingia kwenye skendo wakiwa wamevaa kofia ya Miss Tanzania wasijiangalie wao kama wao, waangalie jamii inayowazunguka.

“Unajua kuna muda mtu unatamani kwenda klabu, na kufanya starehe mbalimbali lakini unaangalia taji ulilolipata ukawakilisha nchi kwa kubeba bendera kwa nini usilitendee haki na kulipa heshima yake? Mimi ninachotaka kusema kuna baadhi ya mastaa wa kike ambao wamepata umaarufu kupitia Miss Tanzania, basi wajirekebishe, wajue njia wanayopita ina miba, kujikwaa si kuanguka na wakiamua kubadilika, nafasi bado ipo wafanye mabadiliko. Nipo tayari kuwasaidia ili wapite njia iliyo sahihi, wawe mfano bora kwa jamii.

Swali: Unazungumziaje mitandao ya kijamii?

Jibu: Mitandao ya kijamii ni mapinduzi ambayo kwa watu ambao si waandishi wa habari, wamepata fursa ya kutoa habari ingawa bila misingi ya habari, ingawa ni njia za mkato. Ni watu wachache wamefanikiwa kutumia fursa hiyo kupata maendeleo, lakini wengi wanaitumia vibaya, kwa Tanzania nathubutu kusema teknolojia hii imepaa sana, imekuja wakati Tanzania bado tunatambaa, ilitakiwa itolewe elimu kwanza ya kutosha kabla ya mapinduzi ya mitandao ya kijamii, ikiwa ni pamoja na kuwekwa sheria kwa yeyote atakayekwenda tofauti.

Mfano, Instagram watu wanatumia bila kufuata maadili hawajui kwamba ina uwezo wa kudhuru kwa zaidi ya miaka 100, watu wanafanya kwa kutukanana, kuchambana, kupatia umaarufu, kuna wakati nilisikia mtu kajiua kisa mitandao ya kijamii. Serikali ingalie kwa jicho la tatu, kuna siku niliona Wakenya wakilalamika Watanzania watolewe kwenye mitandao ya kijami kwa sababu hawajui matumizi yake, ni kweli, sasa hivi mtu akikudai hujamlipa anakuanika katika mitandao ya kijamii, umetofautiana na mtu yanaanikwa kwenye mitandao, Instagram imekuwa kama Mahakama ya kuhukumu wengine.

Mitandao inapaswa ilete maendeleo, mfano familia ya Kim Kadarshian wanatumia mitandao kwa matangazo ya bidhaa zao, lakini kwa Tanzania unakuta ugomvi mkubwa, katikati ndio utaona mtu anasema anauza vitenge, katumia faida ya ugomvi kutangaza bidhaa zake. Nchi saa nyingine inaingia kwenye maruweruwe, kwa ajili ya mtu tu kaamua kuzusha jambo lake kalitupa huko kwenye mtandao wengine wanaamini, au unakuta anaamua kuumiza watu kwa kuzusha vitu vya uongo, nadhani huu ni muda muafaka kwa mamlaka husika kutoa elimu, ili watu wajue sheria zinazolinda matumizi ya mtandao.

Swali: Kwa upande wako mitandao imekuathiri vipi?

Jibu: Mimi nilikuwa sipendi mambo ya mitandao ya kijamii, Meneja wangu ndio amenishawishi sana, sijawahi kuishabikia na nimeingia huko miezi michache, baada ndugu yangu na aliyekuwa rafiki yake kugombana bila sababu nikaingizwa kwenye ugomvi wao. Kile kitendo kiliniuma kiukweli lakini naichukulia kuwa changamoto. Nitakuwa mtetezi wa watu wote watakaoathirika na mtandao, nitalisimamia kidete kuhakikisha watu wanajua haki zao na pale inapotokea wanaumizwa kupitia mitando ya kijamii, nitawasaidia kuhusu nini wafanye kupata haki zao.

Nataka kukomesha wale ambao wamezoea kuumiza wenzao, ili kabla ya kuamua kuchafua wengine, wajiulize kwanza kuhusu hicho anachotaka kukifanya na sheria atakayokabiliana nayo. Siku hizi siri za fa- milia zinahamishiwa kwenye mitandao. Instagram, Twitter, Facebook si baraza, vitu wanavyoandika vinahifadhiwa kwa miaka 100, teknolojia hii nathubutu kusema inavunja urafiki.

Swali: Mumeo ule ugomvi uliohusishwa alichukuliaje, vipi kwa upande wa kazini na familia kwa ujumla?

Jibu: Damu nzito kuliko maji, ule ugomvi ulihusisha ndugu wa familia yangu, sheria ilichukua mkondo, kwa kuwa alitukana pia familia ya watu, nashukuru familia yangu ilikuwa karibu na mimi, mume wangu mwenyewe alisema huyu si mke wangu ninayemjua, ofisini pia nashukuru wamenisapoti. Vijana wengi wameumizwa hawajui pa kuanzia, kupitia mitandao na kipindi changu cha Mimi na Tanzania nimeanza kazi ya kuwasaidia wanaoathirika kwenye mitandao jinsi ya kudai fidia na kupata haki zao.

Ilifika mahali watu wanafeki akaunti, mpaka ya mtoto wangu yupo shule wala hayupo kwenye mtandao, lakini mtu anagoogle anatengeneza akaunti feki na kujifanya anaongea naye, mitandao si sehemu ya kutongozana, kutukanana, ni sehemu ya maendeleo. Badala ya kupoteza muda kukutana sehemu, mnafanya kikao kwenye simu, mnabadilishana mawazo na kuingiza kipato sio kuumizana.

Swali: Ni changamoto gani unakumbana nazo katika maisha?

Jibu: Changamoto kubwa ninayokutana nayo ni muda wa kukaa na familia yangu, muda mwingi nakuwa mbali na familia; mwanangu na mume wangu kwa sababu ya kufanya kazi za jamii. Mimi siiti changamoto naita uamuzi wenye busara kuangalia wapi kwenye uzito. Mume wangu mwanzoni alikuwa mbishi sana hakunielewa, lakini nashukuru imefika mahali alikuja kukubali na kuniacha nifanye kazi. Kitu kingine unapewa habari ukiifuatilia unakuta imebadilika, unafika mahali hata viongozi wa Serikali za mitaa wanaogopa kukupa ushirikiano.

Muda pia unanibana, huku kazi huku niandae vipindi, unakuta nachukua likizo ya wiki mbili ambayo inanifanya nirekodi vipindi 20, ili nipate uwiano wa kutumikia ajira yangu na kazi niliyojipa ya kuitumikia jamii.

Swali: Rubi lini atapata mdogo wake? (Kicheko).

Jibu: Nilitamani kuwa na watoto sita, lakini ukiangalia unachopanga sio anachopanga Mungu. Rubi kila kona nyumbani amepanga midoli, ni alama kuwa anahitaji mdogo wake, muda ukiwadia nadhani mwakani nitamletea mdogo wake, ni shukrani kwa Mungu. Hata hivyo, nina mpango wa kuasili mtoto, mwanzoni nilipata shida kumwambia mume wangu kuhusu hili la kuasili mtoto, nikiogopa asije sema sitaki kuzaa kwa vile naasili, lakini nilishangaa siku nilivyomwambia akasema sawa haina shida.

Sasa Mungu asiponijalia hadi mwakani nitachukua mtoto mmoja au wawili miongoni mwa vituo vya kulelea yatima niwalee kama watoto wangu na kuwapatia mahitaji yote muhimu.

Swali: Unazungumziaje unyanyasaji kwa wanawake?

Jibu: Kama ni jipu basi hilo ni la kuliangalia, elimu endelevu iendelee kutolewa kupinga mila zilizopitwa na wakati, vyombo vya habari na wadau mbalimbali wasiachie Serikali kuanzia ngazi za familia, wakwe, mawifi, jinsi wanavyoishi, hii inatafuna sana jamii. Wanawake wanapigwa hawaendi Polisi, wananyimwa fedha za matumizi, chakula hawapati lakini hathubutu kusema, anaogopa ataachwa.

Swali: Unazungumziaje suala la dawa za kulevya?

Jibu: Maji hufuata mkondo, hizi dawa zisingekuwepo popote vijana wasingekula unga wala mirungi na bangi, wafanyabiashara wa dawa hizo ni kama wauza nguo za mitumba . Mfano Karume pale wapo bize pale kwa vile wanawake wengi wanakatiza pale. Hata wauza unga wanalenga vijana hasa wa maisha bora, vijana wa shule za sekondari, vyuo na wanamuziki.

Kwa kuwa ni biashara inayoendelea kukua, basi vijana wapewe elimu, wapewe mbinu za maisha, hiki kitu kipo, nimeshuhudia wanavyoshushwa kutokana na tamaa ya fedha, Serikali ingesaka njia mbadala ya kuwasaidia vijana kwa kuwapa kazi, wengi wanaingia kwa sababu ya ukata wa maisha na wanahitaji fedha za haraka, rushwa imekithiri nchini.

Vijana wanatoka chuo wana shahada za uzamili, unashangaa hivi inakuwaje tena ameangukia huko, unakuta anasaidiwa atoke lakini anarudi tena, ni kitu gani hicho, wanaokamatwa na dawa za kulevya zitaifishwe zichomwe na wao wafungwe muda mrefu ikiwezekana maisha. Serikali iangalie maslahi ya wananchi na watoto wetu, elimu ianze kutolewa kuanzia shule ya msingi kwa kuwa nguvu kazi kubwa inapotea.

Swali: Una ndoto gani kwa siku za badaye?

Jibu: Ndoto yangu ni kuwa kama Oprah Wilfred ni mtu ambaye ametoka kwenye familia masikini, ukiangalia familia yangu ilikuwa masikini, si kwamba nilibebwa mpaka hapa nilipo ni kwa juhudi zangu binafsi. Oprah ananihamasisha sana, nilikuwa namfuatilia sana mara kuna kipindi anapungua anaiambia jamii, mara mwezi mwingine kaongezeka, anasema. Nilikuja kugundua anajiweka wazi kwa jamii kwa vile ni sehemu yake, natamani na mimi niwe kama yeye.

Swali: Unaweza kueleza historia yako kwa kifupi?

Jibu: Nilizaliwa Arusha mwaka 1978, baba yangu alikuwa askari na tuliishi nyumba ya mabati ndani kumetenganishwa na pazia. Mchana ilikuwa vigumu kulala ndani kutokana na joto la jua, lakini nilivyofikisha miaka mitatu, nilichukuliwa na bibi yangu ambaye niliishi kwake mpaka nilipotimiza miaka minane, kwa vile nilikuwa nazimia na kutokwa damu puani.

Nashukuru kuanzia shule ya msingi nilisoma na kufaulu vizuri hadi kufika kidato cha tano na sita, kiukweli nilipokuja Jangwani nilishangaa he kumbe kuna maisha mengine tofauti na tuliyoishi sisi, ya kuzoa samadi ya ng’ombe, kukata majani, kulisha kuku na kulala nyumba za bati kwa kweli nilishangaa. “Alafu bahati nikawa nasoma na Tulia Akson (Naibu Spika) na Angela Kairuki (Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora) walikuwa chachu kwangu ya mabadiliko nikasema kumbe inawezekana kufika sehemu nzuri zaidi.

Nilisoma kwa bidii sana, kipindi matokeo ya kidato cha sita yanatoka nilifaulu na kupata udhamini wa kwenda kusoma Marekani, nikaondoka nikaenda zangu Marekani na baada ya kurudi niliajiriwa na Standard Chartered Bank. Niliendelea kusoma Chuo cha Diplomasia, nilipomaliza nikajiunga na Chuo Kikuu cha St Augustine, nilisoma Mass Communication na sasa nasoma Shahada ya Uzamivu (PHD) Johanesburg Afrika Kusini. Kwa sasa pia ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasilino cha Umoja wa Mataifa (UN).

WAKULIMA zao la korosho mkoani Lindi wamelipwa Sh bilioni 85 ...

foto
Author: Vicky Kimaro.

Recent Posts

Categories

more headlines in our related posts

latest # news